Ijumaa , 19th Apr , 2019

Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara limewakamata watuhumiwa 21, wanaojihusisha na matukio ya uhalifu ikiwemo uvunjaji wa nyumba na wizi wa pikipiki, ambapo miongoni mwa wahanga wa matukio hayo yumo Mkuu wa wilaya ya Mtwara Evod Mmanda ambaye ameibiwa vitu vyake vya ndani.

Kamanda wa Polisi Mkoani wa Mtwara, Blasius Chatanda-ACP,

Kamanda wa Polisi Mkoani wa Mtwara, Blasius Chatanda-ACP, amesema operesheni hiyo imeanza 01 January 2019 hadi 18 April 2019 ambapo ndani ya kipindi hicho wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 21 wanaojihusisha na matukio ya uhalifu pamoja na mali mbalimbali.

"Katika operesheni inayoendelea Mtwara tumewakamata watuhumiwa 21, pia tumekamata mali mbalimbali zidhaniwazo kuwa za wizi ikiwemo TV 12, Deki 3, Sub wofer 2, kompyuta 7, Solar panel 11 ,mitungi ya gesi 17, pikipiki 7, bajaji moja na zana za uvuvi haramu ikiwemo viroba vitatu vyenye unga unaodhaniwa ni sumu" amesema Kamanda Chatanda.

Aidha, Kamanda Chatanda amesema miongoni mwa wahanga wa uhalifu huo ni Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda ambaye ameibiwa vifaa vya ndani.

"Mkuu wa wilaya ya Mtwara ni miongoni mwa wahanga wa huu uhalifu tulioubaini wakati wa operesheni, yeye ameibiwa vifaa vya ndani ikiwemo TV(Flat Screen)usiku wa 17/04/2019, hawakufanikiwa kuchukua vingine kwakuwa wahalifu hao baadae walikurupushwa ila waliohusika na tukio hili tayari tunao" amesema.

Ameongeza kwamba, "tunawaomba walioibiwa katika matukio mbalimbali, wafike kituo kikuu cha polisi kati mjini Mtwara ili waweze kuzitambua mali zao"

Kamanda Chatanda amesema licha ya mkuu wa wilaya kuibiwa, katika Kompyuta zilizokamatwa pia zimo zilizoibiwa kwenye ofisi za halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.

"Miongoni mwa Kompyuta zilizoibiwa pia zimo ambazo zimeibiwa kwenye Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya  Mtwara Mikindani, tunajiuliza huyu aliyeiba alikuwa na lengo la kuvitumia tu au alikuwa anataka baadhi ya taarifa za ofisi. Watumishi wawili wa Halmashuri wanaotuhumiwa tumewashikilia na tunaendelea na uchunguzi",  amesema Chatanda.