'Mlionipigia kura, hazikutosha' - John Heche

Jumatatu , 2nd Dec , 2019

Mbunge wa Tarime Vijijini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amewashukuru wanachama wenzake waliompigia kura ijapokuwa hazikumpa ushindi, katika kinyang'anyiro cha kumtafuta Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, uchaguzi uliofanyika usiku wa kuamkia leo Desemba 2,

Mbunge wa Tarime Vijijini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche

Katika uchaguzi huo wa ndani Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, aliibuka mshindi kwa kupata kura 44 dhidi ya kura 38 alizopata Mbunge Heche na kumfanya Matiko kuwa Mwenyekiti wa Kanda hiyo.

"Nawashukuru sana wanachama wenzangu na wajumbe kwa kura mlizonipa japo hazikutosha, nawapongeza wengine wote waliotumia Demokrasia yao kuchagua wagombea wenzangu, nawatakia kila la kheri walioshinda katika majukumu magumu mbele yetu" ameandika Mbunge Heche.

Kwa upande wa Kanda ya Kaskazini, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ameibuka mshindi dhidi ya Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, lakini kwa Kanda ya Kusini Seleman Mathew aliibuka kinara, na kwa Kanda ya Nyasa, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa ameibuka kinara pia.