Msafara wa Mbowe wavamiwa na Morani

Ijumaa , 14th Sep , 2018

Msafara wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, umevamiwa na kundi la Morani wakimpokea na kumlaki wakati akiwasili wilayani Monduli mkoani Arusha kwa ajili ya kampeni za Chama chake zinazoendelea katika jimbo hilo leo.

Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe akipokelewa jijini Arusha.

Baada ya kulakiwa Mbowe ametoa hotuba yake kwa wakazi wa Monduli kuwa ifike mahali waachwe washindane kwa hoja na sio siasa za chuki kama ambavyo baadhi ya viongozi wanafanya katika mikutano ya kampeni kwani wote wamepewa mamlaka na wananchi ambao ndio wapiga kura.

Tusihukumiwe kwa tofauti zetu, tusihukumiwe kwa historia zetu, tulumbane kwa hoja”, amesema Mbowe.

Kwa upande wake mgombea wa Ubunge jimbo la Monduli (CHADEMA) Yohana Masiaya amesema kuwa hatolishusha hadhi jimbo la Monduli na kurejesha heshima ya jimbo hilo kulingana na historia yake ikiwemo kuongozwa na Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa.

CHADEMA wanamnadi mgombea wao Yohana Masiaya ambaye anapigania kiti cha Ubunge kwa kupitia jimbo la Monduli ambalo awali lilikuwa likishikiliwa na Mbunge wa CHADEMA, Julius Kalanga kabla ya kujivua Ubunge na kukihama chama hicho kisha kukimbilia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Agosti 4, 2018, tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo matatu ya Monduli, Ukonga na Korogwe Vijijini na wa udiwani katika kata mbili za Tanzania Bara utakaofanyika Septemba 16, mwaka huu, ambapo kampeni zilianza Agosti 21 na zitamalizika kesho Jumamosi Septemba 15.