Jumatatu , 16th Jul , 2018

Baada ya kuwepo na tuhuma za hujuma kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CHADEMA, Iringa kwenda kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi  Kata ya Gangilonga Ndg. Fuad Mwasiposya juu ya kushindwa kupokea fomu za wagombea kwa wakati, Msimamizi huyo amesema anashangaa ni wapi habari hizo zilipotokea -

na kwamba ukweli upo kwenye ripoti yake.

Akizungumza na www.eatv.tv, Ndg. Mwasiposya, amegoma kukubali au kukanusha tuhuma hizo, ambapo kwa mujibu wa maelezo yake amesema kwamba yanayozungumzwa na viongozi wa CHADEMA yeye anaona ni kama hadithi imetungwa na ikandikwa hivyo anaacha iendelee kusimuliwa ili kuleta ladha.

Amesema kwamba laiti kama ingekuwa malalamiko hayo yanatolewa na mgombea mwenyewe kungekuwa afadhali lakini kwa kuwa ni viongozi wengine hawezi kuzungumza na kwamba mgombea anafahamu taratibu zilizopo hivyo ukweli wote utafahamika atakapokabidhi ripoti ya mchakato mzima kwenda kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.

"Mimi siwajibiki na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari, mimi natoa taarifa kwa msimamizi wa Tume ya uchaguzi, kwa mujibu wa utaratibu, nimeshakamilisha zoezi la uteuzi nimekamilisha hatua zote za pingamizi lakini pia uteuz wa mwisho umefanya, Maswali yote hayo unayoniuliza taarifa zipo kwa mamlaka ya juu yangu" Mwasiposya.

Pamoja na hayo, msimamizi huyo wa uchaguzi amesema kwamba anashangaa taarifa hizo kuzungumzwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kwa kuwa anachofahamu kiongozi huyo hayupo Iringa hivyo haelewi maneno hayo ameyatoa wapi.

Kwa upande wa Katibu wa CHADEMA, wilaya Kilolo Jackson Mnyawami amesema kuwa tayari wameshatuma malalamiko yao kama chama kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi jimbo pamoja Mkurugenzi wa Uchaguzi Taifa kutokana na vitendo vinavyofanywa na Wasaidizi wao katika kata.

Akizungumzia suala la fomu zao kutopokelewa amefafanua kuwa, walikwishafanikiwa kumkabidhi fomu hizo Msimamizi huyo wa uchaguzi lakini kilichowashangaza ni kutobandikwa kwenye ubao ili kuweza kutolewa mapingamizi ikiwa ni pamoja na kukataa fomu ya mgombea mmoja akidai siyo ile aliyompatia yeye.

Pamoja na hayo www.eatv.tv, ilipojaribu kumtafuta Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Iringa Ndg. Omary Mkangama juhudi ziligonga mwamba baada ya simu yake kuita kwa muda mrefu pasipo kupokelewa.

Msikilize hapa chini Mwasiposya