Mtafiti wa Sokwe asikitishwa uharibifu mazingira

Monday , 17th Jul , 2017

Mtafiti wa Sokwe katika hifadhi ya Gombe iliyopo Mkoani Kigoma, Dk. Jane Goodall ametaja changamoto kubwa katika uhifadhi wa mazingira ya Gombe kuwa ni kuwepo kwa wakimbizi kutoka Burundi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea kitabu kinachomuelezea Jane Goodall na miaka 50 alioishi Gombe kutoka kwa Mwanaharakati wa masuala ya mazingira na mtafiti wa maisha ya Sokwe katika Hifadhi ya Gombe mkoani Kigoma, Dk. Jane Goodall.

 ambao kwa kiasi kikubwa hushiriki katika shughuli ambazo husababisha uharibu wa mazingira kama vile kilimo na ufugaji usio endelevu.

Aidha, Dk Goodall, ametaja changamoto nyingine kuwa ni uharibifu wa shoroba za wanyama pamoja na makazi yao katika hifadhi ya Gombe na kwamba kwa sasa hifadhi hiyo imezungukwa na maakazi ya binadamu hali iliyosababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa idadi ya wanyama hao.

Mtafiti huyo ametoa kauli hiyo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es salaam

Dk Goodall ambaye anaongoza Taasisi ya Roots and Shoots, amemueleza Mh. Samia kwamba, taasisi yake inachukua hatua mbalimbali katika kupambana na uharibifu wa mazingira katika hifadhi ya Gombe ikiwemo kuhimiza uwepo wa mipango bora ya matumizi ya ardhi.

Amesema, kwa sasa wananchi kutoka vijiji zaidi 52 mkoani wa Kigoma wanapatiwa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira, ambapo jumla ya shilingi Milioni 400 zimekopeshwa kwa wananchi wa vijiji 32 ili kuwawezesha kiuchumi na kushiriki katika miradi ya uhifadhi wa mazingira hususan yenye lengo la kulinda shoroba na makazi ya Sokwe, hatua iliyoanza kuleta mafanikio.

Kwa upande wake Makamu wa Rais amesema, serikali inafanya kazi kubwa katika kuhakikisha mazingira ya hifadhi za Taifa pamoja na ikolojia yake yanatunzwa ambapo amemhakikishia Dk. Goodall kwamba serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuhakiksha wananchi wanafanya shughuli za kujiletea maendeleo bila kuharibu mazingira.

“Ni muhimu kuishirikisha jamii inayoishi pembezoni mwa hifadhi zetu katika suala la uhifadhi wa mazingira lakini pia kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi”, amesema Makamu wa Rais.

Kuhusu suala la wakimbizi kuharibu mazingira, Makamu wa Rais ameahidi kutoa maelekezo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ili kuona namna bora ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Makamu wa Rais amempongeza Dk. Goodall kwa kupewa tuzo ya heshima na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kama ishara ya kutambua mchango wake katika masuala ya uhifadhi wa Sokwe na mazingira kwa ujumla.