Jumanne , 17th Jul , 2018

Mbunge wa Temeke, Mh. Abdallah Mtolea ameweka wazi kwamba  katika Wizara ambazo, zinazofanya kazi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli anavutiwa na wizara ya ardhi kutokana na utendaji  wao pamoja na mikakati yao ambayo imeweza kufanya kazi na kutatua changamoto.

Kushoto ni Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, Kulia ni Waziri wa Ardhi Willium Lukuvi.

Akizungumza na www.eatv.tv, Mtolea amesema kwamba japo changamoto kwa watendaji wa serikali ni nyingi lakini Wizara ya ardhi imekuwa ikijitahidi kupambana nazo.

"Kwa upande wangu wizara inayojitahidi kufanya kazi na zikaonekana ni wizara ya ardhi na makazi. Wizara ile ina mipango na utekelezaji wake unaonekana. Changamoto hazikosekani lakini wamejitolea kupambana kwa hilo mimi naiunga mkono" Mtolea.

Aidha Mtolea amezitaka Wizara nyingine kujifunza kupitia wizara ya ardhi haswa katika suala zima la kufanya kazi kwa vitendo ili kukidhi matakwa ya uhitaji wa watanzania.

Wizara ya Ardhi imekuwa ikiongozwa na Waziri Willium Lukuvi tangu mwaka 2015 baada ya kuteuliwa na Rais John Pombe Magufuli alipoingia madarakani, ambapo amefanikiwa kutatua migogoro mbalimbali ukiwepo mgogoro uliodumu kwa takribani miaka 40 ambapo Mbunge wa Kilwa Kusini Suleiman Bungara 'Bwege' aliutolea ushuhuda kwenye kipindi cha Kikaangoni.