Jumatano , 16th Mei , 2018

Jeshi la Polisi katika wilaya ya Gomba nchini Uganda linachunguza tukio la kuuawa kwa mwanamke mjamzito aliyejulikana kwa jina la Amina Nabukeera (19) katika Kijiji cha Bakandula.

Akisimulia tukio hilo mume wa marehemu Bwana Arafat Kabuubi amesema tukio hilo limetokea jana Mei 15, 2018 muda wa saa mbili usiku wakati akiwa na mkewe wakielekea kununua mahitaji ya nyumbani

“Mimi na mke wangu tulikuwa tunaenda moja ya maeneo ya biashara muda wa saa mbili usiku kununua mahitaji ya nyumbani, nilikua nikitembea mbele yake kabla sijasikia purukushani nyuma yangu na nilipogeuka niliona mtu akimshumbulia mke wangu kwa kumpiga na nyundo kichwani, alimkata sikio la upande wa kulia pamoja na taya kwa kutumia panga kabla ya kukimbia. niliogopa sana na nilikosa nguvu za kumpigania mke wangu” amesema bwana Kabuubi

Bwana Kabuubi aliongeza kuwa alijaribu kupiga kelele za kuomba msaada lakini alikua tayari amechelewa kumuokoa mke wake ambae alifariki wakati akitafuta usafiri wa kumpeleka katika kituo kidogo cha afya.

Mkuu wa Polisi katika mkoa wa Katonga Kamanda Joseph Musana amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuomba wananchi kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa kumbaini mtuhumiwa.

Hilo ni tukio la pili kwa marehemu kushambuliwa ambapo mwezi Machi mwaka huu alishambuliwa akiwa nyumbani kwake lakini alipatiwa matibabu katika kituo kidogo cha afya.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Gomba ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari.