Mwafrika apona Corona, aligoma kurejea nchini kwao

Jumatatu , 17th Feb , 2020

Imeelezwa kuwa Kem Senou Pavel Daryl, ni kijana raia wa Cameroon aliyepatwa na ugonjwa wa homa kali inayosababishwa na virusi vya Corona, alithibitika kupona baada ya kutengwa kwa ajili ya uangalizi maalumu kwa siku 14.

Kem Senou Pavel Daryl, Raia wa Cameroon aliyepona Corona.

Daryly mwenye umri wa miaka 21 anaishi katika Mji wa Jingzhou, amesema kuwa hata baada ya kugundulika kupata maambukizi hayo, hakuwa na mpango wa kuondoka China, hata kama Serikali ya Cameroon ingeshinikiza kuwa hivyo.

Akiwa katika chumba chake cha kupatiwa matibabu alichotengwa kwa siku 14, kijana huyo alisema "Chochote kitakachofanyika sitaki kupeleka ugonjwa Afrika".

Alikuwa anaugua homa kali, kukohoa vibaya na kuonesha dalili za mafua, alitibiwa kwa antibiotiki na dawa za kutibu wagonjwa walio na virusi vya Ukimwi na baada ya wiki mbili ya uangalizi alianza kuonesha dalili ya kupona.

Uchunguzi wa kimatibabu wa CT scan haukuonesha dalili zozote za ugonjwa na kwamba alikuwa mtu wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika aliyepona baada ya kuambukizwa na virusi hatari vya corona na Serikali ya China iligharamia matibabu yake.

Chanzo, BBC Swahili.