Jumamosi , 20th Jul , 2019

Mkuu wa wilaya ya Ilala Sophia Mjema leo Julai 20 amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, ambapo utazunguka na kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika Manispaa hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Ilala Sophia Mjema na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo wakikabidhiana Mwenge.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Chongolo amesema, Mwenge huo utakagua miradi mbalimbali takribani 8.

''Nakiri kuupokea  Mwenge wa Uhuru mwaka 2019,  kutoka kwa dada yangu Sophia Mjema, ukiwa unawaka unang'aa na unameremeta, utatembea umbali wa km 62 na  miradi 8 yenye thamani ya Shilingi bilioni 80.76 itazinduliwa'' amesema Chongolo.

Mwenge huo wa Uhuru mwaka huu umebeba ujumbe usemao ''Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa''.

Mwenge wa Uhuru uliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalim Julius Nyerere, ambapo uliwashwa rasmi  uliwashwa kwa mara ya kwanza Decemba 9, 1961 na kupandishwa juu ya  mlima Kilimanjaro, ili uweze kumlika nje na ndani ya mipaka yetu, na kuleta matumaini ambako hakuna matumaini, upendo ambako kuna chuki.