"Mwenye ndugu jambazi aende Muhimbili" - Mambosasa

Jumatatu , 25th Mei , 2020

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa, amewataka wale watu ambao wana ndugu zao majambazi na wanajua kabisa walienda kutafuta lakini hawajarudi, basi waende Muhimbili kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa.

Hayo ameyabainisha leo Mei 25, 2020, wakati akitoa taarifa za majambazi saba waliouawa wakati wa majibizano ya risasi na Polisi usiku wa kuamkia leo, waliokuwa wakielekea kufanya ujambazi katika ghala la GS Group Limited, ambapo kwa bahati mbaya majambazi hao majina yao hayakuweza kufahamika.

"Kama unavyoelewa hakukuwa na mahojiano kati ya Jeshi la Polisi na wahusika, walipoona wanafuatiliwa walianza kukimbia, walianza kusalimia kwa kurusha risasi na Askari wakajibu, mpaka sasa sina majina ya wahusika lakini mtu yeyote anaweza kwenda Muhimbili kwa ajili ya kutafuta kama anajua, kuna ndugu yake jambazi haonekani alienda kuvuna ameshindwa kurudi, basi aende Muhimbili ataweza kumtambua ndugu yake" amesema Kamanda Mambosasa.