Jumatatu , 14th Mei , 2018

Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza jeshi la Polisi nchini kuruhusu taasisi za dini kufanya mikutano yao pindi watakapoomba kibali.

Akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na Kanisa la Waadventista Wasabato jijini Mwanza, Dk Mwigulu amesema kuwa mafundisho yanayotolewa na taasisi za dini yanasaidia kuwa na jamii yenye raia wema.

Dk. Nchemba amesema ni lazima kuheshimu uhuru wa kuabudu wa kila dini uzingatiwe kwa kuruhusu wanafunzi na wafanyakazi kwenda sehemu zao za kuabudu kama ilivyopangwa.

Aidha ameongeza kwamba kwa kuwa Wizara hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia uhuru wa kuabudu, watahakikisha wanazungumza na mashirika  na hata shule ambazo zinawazuia wanafunzi na wafanyakazi kuhudhuria kwenye ibada siku za jumamosi.

‘’Nimeagiza jeshi la Polisi wawape uhuru wa kuabudu kwa sababu mnatengeneza jamii iliyobora lakini pia tutazungumza na wahusika kwenye taasisi za elimu na ajira ili tutoe maamuzi yatakayotolewa yasilete doa kwani kazi hii inasaidia kunyoosha nchi,’’  Dk Mwigulu.