Jumamosi , 12th Sep , 2020

'Vijiweni ama vijiwe' ni sehemu maarufu kwa wanaume kupiga soga, kuzungumza na kubadilishana mawazo huku wakiwa ama wanakunywa vinjwaji, wanacheza bao, draft au ni sehemu ya ofisi ya ufundi n.k. 

Vijana wakicheza draft katika 'kijiwe'

Mazungumzo ya vijiweni aghalabu huegemea zaidi na wakati husika, mfano katika kampeni mazungumzo mengi ambayo hutawala huwa ni ya siasa, kama ilivyo kwa wakati huu ambao nchi inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu, Oktoba 28.

Katika kipindi hiki cha kampeni majukwaa mbalimbali ya kisiasa yamekuwa yakitumiwa na wagombea katika kujinadi na kuelezea sera zao, lakini hilo hufanyika pia katika vijiwe ambapo wasiokuwa na vyama na wanachama wa vyama tofauti hukutana katika vijiwe hivi ili kujadili, kuelezeana kinagaubaga, kushawishiana pamoja na kutafakari yale yanayoongelewa katika vizimba na majukwaa ya kisiasa.

''Watu wengi wanaofanya masuala ya kujadiliana kwenye vijiwe wanakuwa wanajuana sana, mbali na siasa kufanyika kwenye majukwaa, Sio wote wanaopata fursa ya kwenda katika mikutano ya kisiasa hivyo wanaokwenda wachache wanakuja kwenye vijiwe na kuwambia wenzao kinachokuwa kimejiri huko, mimi kwa upande wangu bado naona hivi vijiwe vina nafasi kubwa sana ya kutoa maarifa'', Said Nguya, Mchambuzi wa Siasa.

Aidha Nguya anaamini kuwa suala la kufahamiana miongoni mwa watu wanaopendelea kukaa vijiweni, huwafanya wahusika kuwa huru kujadiliana pamoja na kujuana katika uwezo wa kujenga na kuwasilisha hoja miongoni mwao, pia kutambuana nani anaweza kuaminika katika utoaji wa taarifa na mawazo mbalimbali wawapo vijiweni.