"Nafasi zenyewe chache, Ubunge wa nini" - Waitara

Jumapili , 5th Jul , 2020

Naibu Waziri wa TAMISEMI Mwita Waitara, amesema kuwa kama yeye angelikuwa ni Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa basi asingehangaika kutafuta nafasi ya kugombea Ubunge, kwani angeridhika na nafasi yake aliyokuwa nayo.

Naibu Waziri wa TAMISEMI Mwita Waitara.

Waitara ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kusema kuwa kauli ya Rais Magufuli ya kuwataka wateule wake kuridhika na nafasi walizonazo, iko sahihi kabisa kwa kuwa nafasi za kuteuliwa ni chache sana na ni jambo la kumshukuru Mungu.

"Unajua hizi nafasi za kuteuliwa siyo nyingi sana, kwa mfano wewe ni RC, unakuwa ndiyo Mwenyekiti na Mkoa wako labda una Wabunge 11, kwahiyo unakuwa unaongoza Wabunge 11, unasema unaacha u-RC eti unautafuta Ubunge, kama mimi ningekuwa RC ningebaki na Ukuu wa Mkoa wangu kwanza tuko wengi nafasi zenyewe ni chache, kama umepewa nafasi hiyo kwanini usiikamilishe" amesema Waitara.

Hivi karibuni Rais Magufuli wakati akiwaapisha viongozi aliowateua, Ikulu ya Dar es Salaam, aliwasisitiza umuhimu wa kuridhika na nafasi walizonazo, kwani kutoridhika na nafasi zao kuna sababisha migogoro isiyokuwa na tija miongoni mwao wao wenyewe.