Alhamisi , 18th Apr , 2019

Naibu Spika wa Bunge, Dkt Tulia Ackson ameagiza hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, iliyokuwa ikisomwa na Mbuge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, kutohifadhiwa kwenye kumbukumbu za Bunge baada ya Mbunge huyo kugoma kuisoma.

Mbunge Sugu alishindwa kusoma hotuba hiyo kufuatia kile alichokilalamikia kuwa asilimia kubwa ya maneno yaliyokuwa kwenye hotuba hiyo kuondolewa kwenye hotuba yake.

Kufuatia malalamiko ya Sugu, Naibu Spika Dkt Tulia alimtaka Mbunge huyo kusoma hotuba ambayo imewasilishwa Bungeni na wabunge wengine wanayo.

Kufuatia sintofahamu hiyo, Mbunge huyo wa Mbeya Mjini alilazimika kutoisoma hotuba hiyo ya bajeti mbadala baada ya sintofahamu ya muda mrefu.

Naibu Spika Tulia Ackson na Mbunge Joseph Mbilinyi wamekuwa wakitajwa mara kwa mara huenda wakawa washindani wakubwa kuelekea uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020, endapo kila mmoja ataonesha nia ya kuwania Ubunge kwenye jimbo hilo.