Jumamosi , 12th Oct , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, amesema kuwa hatasita kuwachukulia hatua viongozi wa mikoa na wilaya ambao watashindwa kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kupigia kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Rais Magufuli

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2019, mkoani Katavi, alipokuwa akihutubia wananchi kwenye uwanja wa ndege wa Mpanda, ambako amezindua safari za ndege za ATCL katika uwanja huo.

'Jana Waziri wa TAMISEMI alitoa takwimu kwa mikoa na wilaya ambazo zimefanya vizuri kwenye kuhamasisha watu kujiandikisha, nasubiri zoezi limalizike na kwa viongozi ambao mikoa na wilaya zao zitafanya vibaya najua watanzania hawatanilaumu kwa hatua nitakazochukua kwa viongozi' - Rais Magufuli.

Rais Magufuli akaongeza kwa kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Katavi kwenda kujiandikisha ili kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo. 'Kama hapa Katavi mpo watu ambao hamjajiandikisha, nendeni mkafanye hivyo'.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameeleza hatua zilizofikiwa mpaka sasa baada ya kutoa msamaha kwa washtakiwa wa uhujumu uchumi kwa sharti la kukiri na kurejesha fedha walizoiba. 

'Leo nimezungumza na DPP, amenieleza kuwa mpaka sasa watu 138, waliokuwa wameiba mabilioni ya fedha, wamejitokeza na kuomba msamaha na wameshalipa fedha hizo na tayari wameachiwa huru' - Rais Magufuli.