Alhamisi , 16th Mar , 2017

Kampuni ya East Africa Television Limited kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki za Wanawake  (HAWA) imefanikiwa kuwasitiri  wanafunzi 673 kwa kuwapatia pedi za kujisitiri kipindi cha hedhi kupitia kampeni ya 'Namthamini'.

Kutoka kushoto, Sophie Proches Mratibu wa Vipindi EATV, Basilisa Biseko Afisa masoko EATV Ltd, Joyce Kiria Mkurugenzi HAWA Foundation na Mratibu wa vipindi EA Radio, Irene Tillya

Kampeni hiyo ilikuwa ikiendeshwa kwa takriban siku 8 kupitia EATV na East Africa Radio, ikiwa na lengo la kusaidia wanafunzi wa kike waweze kuhudhuria masomo yao shuleni bila kukosa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Akizungumza leo na wanahabari Afisa Masoko wa kampuni hiyo Bi. Basilisa Biseko amesema kuwa katika kampeni hiyo wamefanikiwa kukusanya  jumla ya shilingi 20,176,110/ (Zaidi ya shilingi milioni 20.176) ambapo pesa taslimu ni shilingi 11,774,610 (Milioni 11.774) huku thamani ya pedi zilizopokelewa ikiwa ni sh 8,401,500 (milioni 8.401) kutoka kwa wadau mbalimbali.

Bi. Biseko akiwakilisha EATV pamoja EARadio amesema hata baada ya kampeni hiyo kumalizika, wananchi wanapaswa kuwa mabalozi katika kuhakikisha msichana kwenye jamii anasitiriwa na kuthaminiwa kwa kupatiwa vifaa wakati wa hedhi pia kupatiwa elimu juu ya hedhi salama.

Basilisa Biseko, Afisa Masoko EATV Ltd

"Sisi kama EATV Limited hatuwezi kumaliza tatizo hili peke yetu, tulidhamiria kusaidia wanafunzi 1500 lakini tumefanikiwa kwa wanafunzi 673, tunaomba iwe chachu katika jamii kwani jukumu hili ni la kwetu sote kuhakikisha hakuna binti anayekosa kwenda shule kwa kukosa vifaa vya kujisitiria wakati wa hedhi. Tuendelee kuwasaidia watoto wa kike kupata mahitaji uhimu wawapo mashuleni". Bi Biseko alizidi kusisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya  HAWA , Bi. Joyce Kiria amesema wadau wengi wanaohusika na masuala ya kuwasaidia wanawake kwa kipindi kirefu walikuwa na ndoto ya kupata misaada kupitia vyombo vya habari hivyo kampuni ya East Africa TV kuendesha kampeni ya 'Namthamini' moja kwa moja imekuza uelewa kwa kiasi kikubwa katika jamii.

Bi. Kiria ameongeza kuwa taasisi ya HAWA na taasisi nyingine zinazojishughulisha na masuala ya wanawake hawataendelea kubweteka bali watazidi kuendelea kupambana kuwasaidia mabinti na kuongeza kuwa katika jukumu hilo wabunge pamoja na viongozi wengine waendelee kusaidiana na jamii kumjali na kumthamini mwanafunzi wa kike.

Wanafunzi wa kike darasani katika moja ya shule za msingi nchini Tanzania

"Wabunge na viongozi mbalilmbali mliopata nafasi ya kushiriki katika kampeni mlitusaidia kukuza uelewa lakini mkatusaidie kupaza sauti zaidi, Kama tunaweza kukuta kondomu sehemu mabalimbali na zinatolewa bure, au watu wanapatiwa bure, basi inatakiwa hata pedi za bure zitolewe au zipatikane kwa bei rahisi ambayo kila mtu ataweza kuhimili gharama". Kiria alimaliza.

Sanjari na hayo Bi. Biseko amemalizia kwa kusema kwamba michango yote iliyokusanywa itapelekwa katika shule ishirini zipatikanazo kwenye mikoa mitano ya Tanzania ambayo ni Morogoro, Iringa, Lindi, Pwani na Tanga.

Kutoka kushoto ni Basilisa Biseko, Joyce Kiria na Mratibu wa vipindi EA Radio, Irene Tillya

Namthamini ni kampeni iliyokuwa inahamasisha uchangiaji wa pedi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaotokea katika mazingira magumu iliyoanzishwa na kampuni ya East Africa TV iliyoenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.