Jumatatu , 24th Sep , 2018

Baada ya Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye kupata ajali ya gari asubuhi ya leo Septemba 24, 2018, ameibuka na kuwashukuru wananchi wa kijiji cha Kibutuka Wilayani Liwale pamoja na wote waliomtakia heri.

Kushoto ni picha za ajali na kulia ni Nape Nnauye

Nape amesema wananchi wa Kibutuka walifika eneo la ajali na kuwasaidia kuwatoa ndani ya gari pia wakawasaidia kulisukuma gari kwenda kulihifadhi katika kituo cha afya cha Kibutuka.

Ajali hiyo ilihuisha gari lake alilokuwa akilitumia aina ya Land Cruiser VX (nyeupe) lenye namba za usajili T349 DEL, ambalo liliacha barabara na kupinduka.

Nape alipata ajali hiyo akiwa anaelekea wilayani Liwale kuungana na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Taifa Dkt. Bashiru Ally anayezuru wilayani Liwale

Hata hivyo ajali hiyo haikuwa na madhara makubwa yaliyotokea kwa waliokuwa ndani  ya gari. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Lindi Renatha Mzinga alisema, eneo ilipotokea ajali hakukuwa na tatizo lolote hivyo uchunguzi zaidi unaendelea.