Ijumaa , 17th Aug , 2018

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, amesema ipo haja ya kupitiwa upya kwa sheria inayosimamia thamani ya kura hasa katika kipindi hiki cha wabunge na madiwani kuhama vyama vyao.

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye.

Nape amesema kuwa  ni vyema kukawa na sheria ambayo itampa mamlaka mbunge au diwani anayehama chama baada ya uchaguzi, aendelee kuwa na nafasi hizo katika chama anachokwenda ili kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika katika chaguzi ndogo kwenye maeneo ambayo mbunge au diwani amehamia chama kingine.

Ametoa kauli hiyo akiwa kwenye ofisi ndogo za Bunge visiwani Zanzibar, katika mafunzo ya siku mbili ya kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge pamoja na wajumbe wa tume ya utumishi wa Bunge ambapo amesema pamoja na uwepo wa wimbi kubwa la wanasiasa kuhama, wapigakura wanatakiwa kupewa thamani yao kwa kuwa wakati wa uchaguzi wao ndio uhitajika kupiga kura kuchagua wawakilishi wao.

"Siwezi kupingana na Katiba kuhusu hamahama za wanasiasa lakini ni vyema thamani ya wapiga kura ikatambulika vyema, bado thamani ya mpiga kura inapaswa kuenziwa,” amesema Nape.

Wakati hayo yakijiri Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally anatarajiwa kufanya  ziara ya kikazi ya siku nne visiwani humo kuanzia leo  Agosti 17 hadi 20 mwaka huu. 

Dk.Bashiru anafanya ziara hiyo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo Mei mwaka huu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Abdulrahman Omar Kinana kustaafu.