Alhamisi , 21st Mar , 2019

Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari, amesema kuwa hakuna taarifa yoyote inayosema kuwa amerejeshewa ubunge na tayari shauri liko Mahakamani linalozuia jimbo lake kufanyiwa uchaguzi.

Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari.

Akizungumza na www.eatv.tv, Nassari amesema kuwa taarifa zinazoenezwa ni uzushi na hakuna taarifa yoyote rasmi ambayo amefikishiwa kuhusu hilo.

"Taarifa iliyopo ni Machi 18, 2019 ndiyo nilifungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kupinga hatua ya Spika kunivua ubunge", amesema Nassari.

Aidha akizungumzia tuhuma za kuwa yuko mbioni kujiunga na chama tawala (CCM),     Nassari amesema kuwa hakuna kitu kama hicho, ni taarifa za uzushi kwa sasa yuko katika harakati za kutetea uwakilishi wake kwa wananchi wa Arumeru.

Mapema leo ziliibuka tetesi kupitia mitandao ya kijamii zilizodai kuwa kiongozi huyo amesamehewa na Bunge, kutokana na kuonekana kupoteza sifa za kuendelea kuwa Mbunge baada ya kukosa vikao vya mikutano mitatu ya bunge bila taarifa.