Jumanne , 12th Feb , 2019

Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Meru mkoani Arusha kimelalamikia kutoonekana kwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kwa zaidi ya miaka 2 na kueleza kutokuwa na taarifa yoyote kiongozi huyo yuko wapi.

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM wilayani humo,Simon Kaaya, wanalazimika kufanya kazi za Mbunge huyo licha ya kutokuwepo katika mikutano ya Bunge kwa kipindi kirefu.

Akizungumza Jijini Arusha Simon Kaaya amesema, "tunajua mheshimiwa Lissu alikuwa anaugua na yuko nje ya nchi kwa matibabu lakini kuna kijana mwingine, Joshua Nassari ambaye hatujui yuko wapi Bungeni hayupo, jimboni hayupo huu sasa ni mwaka wa pili lakini sijamsikia Spika akitoa mwongozo tunamuomba Spika atusaidie."

Mara kwa mara Joshua Nassari amekuwa haonekani lakini kupitia chama chake walishawahi kueleza kiongozi huyo alikuwa akimalizia masomo yake nje ya nchi.

Lakini kupitia ukurasa wake rasmi wa instagram, Joshua Nassari mara ya mwisho alipost picha Januari 27 mwaka huu akiwa na moja ya viongozi kutoka nchini Kenya Raila Odinga lakini hakubainisha ni wapi alipokuwa.