Jumanne , 25th Jun , 2019

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ameitaka serikali kutoa tamko kufuatia kauli yenye kuashiria ubaguzi aliyoitoa mmoja wa wabunge wa Kenya.

Spika Ndugai na Jaguar

Amesema hayo kufuatia kusambaa kwa video mtandaoni ikimuonesha Mbunge wa Jimbo la Starehe nchini Kenya, Charles Njagua Kanyi 'Jaguar', akitishia usalama wa wageni mbalimbali wanaofanya kazi pamoja na biashara nchini humo.

Leo Jumanne, Juni 25, Mbunge wa Rufiji-CCM, Mohammed Mchengerwa amehoji bungeni juu ya umuhimu wa Serikali kutoa ulinzi kwa Watanzania wanaoishi, kufanya kazi pamoja na biashara nchini Kenya, ndipo Spika Ndugai alipotoa rai hiyo kwa serikali.

"Ninaiomba Serikali kutoa tamko hii leo kufuatia kitendo hiki", amesema Spika Ndugai.

Katika video hiyo inayosambaa kwa kasi, Mbunge Jaguar amesema, "hapa hatuwazungumzii wachina 6, tunawazungumzia mamia ya wageni wanaofanya kazi hapa. Ninaipa serikali masaa 24 kuwaondoa hawa wageni, endapo itashindwa, nikiwa kama mwakilishi wa eneo hili, tutakwenda katika maduka, tutawapiga na kuwafurusha hadi uwanja wa ndege ili warejeshwe walikotoka".

Kauli hiyo ya Jaguar imewalenga zaidi raia wa Tanzania na Uganda, ambao kwa madai yake ndiyo waliochukua fursa zao za kibiashara nchini humo.

Baada ya viongozi mbalimbali kutoa matamko yao kuhusu video hiyo wakiwemo mabalozi wa Kenya na Tanzania pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jaguar aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa hakukusudia raia wa Tanzania na Uganda, bali aliwakusudia Wachina ambao wamepora fursa zao za kibiashara.