Ndugu wagoma kuchukua mwili wa Akwilina

Jumatatu , 19th Feb , 2018

Ndugu wa mwanafunzi wa Chuo cha NIT, Akwilina Akwilini ambaye amefariki kwa kupigwa risasi Februari 16, 2018 wamegoma kuchukua mwili wa mwanafunzi huo kwa kile kilichodaiwa kuwa wanahitaji ripoti kamili ya kifo chake.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mhandisi. Profesa Zacharia Mganilwa amethibitisha hilo na kusema kuwa ndugu wanaendelea kujadiliana kuona jinsi gani wanaweza kupokea mwili huo wa mpendwa wao.

"Ripoti juu ya kifo chake madaktari wanasema itakuwa tayari baada ya siku 14 hivyo wakawa wamewaruhusu ndugu kuchukua mwili huo ili wakazike lakini ndugu wa marehemu wanasema hawawezi kuchukua mwili mpaka wajue yaani ripoti itoke ndiyo waweze kuchukua mwili kwa hiyo bado wanaendelea kufanya majadiliano na mamlaka husika" alisema Profesa Zacharia 

Baada ya ndugu kususia mwili wa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Akwiline, Mochwari ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imetoa majibu ya uchunguzi wa kifo chake, baada ya hapo ndugu waliweza kuchukua mwili huo na kuhifadhi tena mochwari Muhimbili huku wakifanya maandalizi ya mazishi. 

Mnamo Februari 16, 2018 Akwilina alipigwa risasi akiwa kwenye daladala ambayo inasemekana ilikuwa inapita eneo ambalo polisi walikuwa wakiwatawanya wafuasi wa CHADEMA ambao walikuwa wakielekea kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi Kinondoni.