Jumatano , 13th Mar , 2019

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF Prof. Ibrahim Lipumba amesema kwamba baada ya kupitia kwenye mapito ya muda mrefu ndani ya chama hicho amekuwa imara zaidi.

Prof. Lipumba mwenye shati lenye rangi nyekundu

Akizungumza katika Mkutano wa uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho  unaofanyika katika ukumbi wa Lekam huko Buguruni, Jijini Dar es salaam, Lipumba amesema kwamba akipatiwa nafasi ya Uenyekiti kwa sasa atakuwa imara kuliko awali kwa kuwa amepitia kwenye moto.

Akijibu swali la kukifikisha chama salama na yeye akiwa Nahodha, Lipumba amesema atashirikiana na bodi ya wadhamini wa CUF kuhakikisha wanashughulikia kesi zilizofunguliwa na bodi feki.

"Pana bodi ya udhamini moja, Chama cha CUF kimoja, naombeni kura zenu tujenge chama imara. Tumepita katika mgogoro kama moto. Chuma ukikipitisha kwenye moto kina kuwa imara zaidi na Lipumba akitoka kwenye moto huo anakuwa ngangari kinoma kweli kweli", amesema Lipumba.

Katika uchaguzi huo mgombea mwingine ni Diana Simba, ambaye yeye amesema si kwamba Lipumba ndiye msomi pekee  kwani hata yeye ana Stashahada ya Maendeleo ya Jamii hivyo anaamini anaweza kukiongoza chama hicho.

Diana  ni mwanamke pekee anayegombea nafasi hiyo.

CUF upande wa Lipumba, wanafanya uchaguzi huku kukiwa na mgogoro ambapo CUF upande unaomsapoti Katibu Mkuu wa Chama hicho wakipingana na mkutano huo kwa madai kwamba Lipumba hana uhalali wa kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho tangu alipotangaza kujivua nafasi hiyo 2015.