Jumatatu , 13th Jul , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi amesema kuwa hana mpango wa kugombea Ubunge, kwani akiwa Mbunge itamulazimu kupeleka shida za wananchi wake kwa Mkuu wa Mkoa ili amtatulie, kitendo ambacho hayuko tayari kukifanya.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi.

Hapi ametoa kauli hiyo hivi karibuni, wakati akifanya mahojiano maalum na EATV na kusema kuwa mara nyingi amekuwa akitajwa na watu kwamba atagombea Ubunge, na kusema kuwa dhamana aliyopewa na Mungu kupitia Rais Magufuli ni kubwa, hivyo anao wajibu wa kuendelea kuwatumikia wananchi.

"Sioni kama kukimbilia kwenye Ubunge ni uamuzi sahihi sana, Mimi nina Wabunge 11, wakiwa na shida wanakuja kwangu, sasa mimi ninapokimbia Ukuu wa Mkoa niende kwenye Ubunge ili na mimi niwe napeleka shida kwa RC ni kitu ambacho kidogo hakiingii akilini, wananchi waendelee kuniombea na wawe na subra huko mbeleni Mungu akijalia na umri ukiwa umesogea tunaweza kwenda eneo hilo" amesema Hapi.

Aidha Hapi amewataka wanasiasa kuwa na heshima badala ya kuendelea kulaumu kwa kila kitu na kufuata sheria na taratibu hususani katika masuala ya ufanyaji wa mikutano.