Jumapili , 31st Mar , 2019

Ikiwa yamepita masaa kadhaa tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kumkosoa Mchekeshaji aliyejizolea umaarufu kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao, Pierre Maarufu kama Mzee wa Liquid hatimaye ameanza kupata mashavu ikiwepo wilayani Kisarawe na Jiji la London, Uingereza.

Pierre

Katika hafla iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo yenye malengo ya kutokomeza Zero katika wilayani humo, Makonda alisema kwamba watu wa 'hovyo' kama Pierre hawapaswi kupewa nafasi kwenye vyombo vya habari.

"Wakina mama kama hawa wanaojituma na kuhangaika kwa ajili ya watoto, wao ndio tuwape kipaumbele, sio hawa walevi walevi, yaani unakuwa na taifa ambalo watu wa hovyo ndio wanakuwa maarufu”, Paul Makonda.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya Jokate kupitia ukurasa wake Instagram amemuomba Radhi Pierre na kumkaribisha Kisarawe ikiwa ni pamoja na kumpatia fursa ya kutengeneza samani za shule mpya inayotegemewa kujengwa katika Wilaya hiyo.

"Nimesikia ni mtengeneza mzuri sana wa 'furniture'. Hii Shule tunayoenda kujenga inahitaji madawati. Naomba tufanye kazi na wewe katika hii fursa. Tuangalie namna japo kidogo tukuwezeshe.  Tunasema Karibu Kisarawe ukae. Kisarawe Kunogile. Tunasema Samahani kwa kukwazika lakini zaidi Asante Sana kwa kushiriki", ameandika Jokate .

Mh. Jokate ameongeza kuwa, "kipekee kabisa nimshukuru Pierre Liquid, wako watu maarufu wengi mno tuliowaalika lakini hawakufika. Ila wewe ulichukua muda wako kuhamamisha na kufika na zaidi ya hapo ukatoa mchango wa Tsh. Laki moja!!!. Hukuja kuuza sura tu!!. Nasema asante sana" Mh. Jokate

Mbali na dili la Mh. Jokate, Mchezaji wa kulipwa wa klabu ya Tottenham Hotspur F.C. raia wa Kenya, Victor Wanyama amemtaka Pierre aende London yeye na msanii Ommy Dimpoz kwa ajili ya matembezi huku akiahidi kugharamia safari nzima.

Ukiachilia mbali mashavu hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla naye ametaka Pierre aheshimiwe utu wake na kwamba ni mtu huru kwenye nchi yake.

"Jamani maisha ni magumu, yana mitihani mingi na ni mafupi sana. Katika kuleta furaha na shangwe kwenye maisha ndiyo maana ‘wachekeshaji’ wakapata ajira!. Wengine tusome udaktari, uhandisi na tufanye uvumbuzi na utatuzi wa changamoto na wengine watutetemeshe, watuvuruge akili, watupe raha na furaha, watuchekeshe, siku zisogee", amesema Kigwangalla katika ujumbe wake.

Ameongeza kwamba, "Maisha ndiyo haya haya! Zaidi ya yote, Pierre ni mtu huru kwenye nchi yake. Tunapaswa kuulinda uhuru wa Pierre kama ambavyo Katiba ya nchi yetu inavyoelekeza. Let him be. Tumuache apate riziki yake. Mungu anajua zaidi kwa nini hatukumjua miaka 5 iliyopita na kwa nini sasa anazua mjadala".