
Katika kesi ya msingi, Mariam Kasembe anadai kuwa alidhalilishwa na mbunge huyo wakati wa kampeni za uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka jana.
Jaji aliyekuwa akisikiliza pingamizi hilo, Dkt. Fauz Twaibu, ameeleza mahakamani hapo baada ya kusikiliza maelezo kutoka pande zote mbili kwamba maamuzi yatatolewa muda huo baada ya kujiridhisha kwa kupitia maelezo yaliyotolewa na pande zote.
Katika kesi hiyo Kasembe anasimamiwa na mawakili watatu,wakiongozwa na Elphace Rweshabura toka kampuni ya mawakili ya Derost Attorneys huku Mwambe akisimamiwa na wakili wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Wakati wa usikilizaji wa madai hayo, Tundu Lissu aliyeanza kuongea mfululizo kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana aliieleza mahakama kuwa hati ya maombi haijatamka vifungu vya sheria vinavyoipa mamlaka mahakama ya kusikiliza shauri hilo na kuwa ina mapungufu kadhaa, hivyo inatosha kuliondoa shauri hilo mahakamani hapo.
Kwa upande wake, wakili Elphace Rweshabura aliieleza mahakama kuwa sio kweli kwamba tuhuma haziko wazi na kwamba mtuhumiwa anajua kesi yake ni nini na alitenda akiwa wapi.