Jumatano , 20th Mar , 2019

Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), Wilaya ya Shinyanga Mjini, limelitaka Jeshi la Polisi kutoingilia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa baraza hilo, kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na ule wa marudio katika kata na majimbo mbalimbali, jeshi hilo lilikuwa likiingilia uchaguzi huo mara kwa mara.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Shinyanga, Mwenyekiti wa BAVICHA Wilaya ya Shinyanga Mjini, Samson Ng’wagi, ambapo ameliomba jeshi hilo kuviacha vyama vishindane.

“Tunaliomba Jeshi la Polisi lisitumike kisiasa na kukipendelea chama tawala bali lifanye kazi yake ya kulinda amani na lisiwe sehemu ya chanzo cha vurugu. Lituache sisi wanasiasa tushindane kwa hoja majukwaani”, amesema Ng’wagi.

Aidha Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa, “sisi CHADEMA huwa tunachukizwa sana pale tunapoliona jeshi letu ambalo ndiyo tunalitegemea kulinda usalama wa raia kuwa sehemu ya wanasiasa".