Jumanne , 4th Feb , 2020

Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime, amewataka Watanzania kuwa na subra kwani uchunguzi wa tukio la vifo vya watu 20, vilivyotokea Mjini Moshi, bado unaendelea, licha ya Mtume Mwamposa pamoja na wenzake saba kuachiwa kwa dhamana.

Msemaji wa Jeshi la Polisi ACP David Misime na Mtume Mwamposa

Katika taarifa yake leo Februari 4, 2020, ACP Misime, amesema kuwa, Mtume Mwamposa pamoja na wenzake wameachiwa kwa mujibu wa kanuni na sheria na kwamba uchunguzi utakapokamilika Watanzania watajulishwa.

"Katika uchunguzi huo walikamatwa watu Nane akiwepo Mwamposa na kuhojiwa kwa kina na baada ya kujiridhisha na yale yaliyokuwa yanahitajika kutoka kwao, wamepewa dhamana kwa mujibu wa sheria ili waendelee kuripoti wakati uchunguzi ukiendelea na ukikamilika yatakayobainika yatatolewa kwa mamlaka husika na kutekelezwa" amesema ACP Misime.

Miili ya watu 20 walioaga dunia baada ya kukanyagana, wakati wakigombea kukanyaga mafuta ya upako siku ya Februari 1, katika kongamano la Mtume Mwamposa, iliagwa jana Februari 3, 2020, katika viwanja vya Mashujaa Mjini Moshi.