Ijumaa , 14th Dec , 2018

Rais John Magufuli amefuta maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Elimu yanayoelekeza Nembo na Wimbo wa Taifa kutumika kwenye dhifa za kitaifa pekee, ambayo pia yanaelekeza kuwa rangi ya njano katika Bendera ya taifa inatakiwa kuwa rangi ya dhahabu badala ya njano ya sasa.

Rais, Dkt. Magufuli.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu na Gerson Msigwa imesema kuwa barua hiyo iliyotolewa na Wizara ya Elimu inaathiri uzalendo wa Watanzania na inaleta mkanganyiko wa tafsiri ya rangi na alama zilizomo kwenye bendera ya Taifa.

"Barua hiyo yenye kichwa cha habari, 'MATUMIZI SAHIHI YA BENDERA, NEMBO NA WIMBO WA TAIFA' imetoa maelekezo ambayo hata mimi mwenyewe tangu nasoma shule hadi leo nafahamu kuwa bendera ya taifa ina rangi ya njano na sio ya dhahabu, na rangi hiyo ya njano inawakilisha madini yote na sio dhahabu peke yake", amesema Rais Magufuli kwenye taarifa hiyo ya Ikulu.

Ameongeza kuwa, "Kwahiyo nimeamua kuifuta barua hiyo na kama kuna mabadiliko basi ni lazima yafanyike kwa kuzingatia taratibu zote kwa kuwa jambo hili ni la kitaifa na sio la mtu mmoja," ameongeza Rais Magufuli.

Hayo yanajiri kukiwa na sintofahamu juu ya kusambaa kwa barua mitandaoni,  ambayo imeandikwa Novemba 23 mwaka huu ikiwa na kumbukumbu namba CHA-56/193/02/16, ambayo inasema wizara hiyo imepokea barua ya maelekezo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuhusu matumizi sahihi ya bendera na Nembo ya Taifa, na Wimbo wa Taifa.