Jumatatu , 14th Oct , 2019

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amesema moja ya vitu ambavyo Mwalimu Nyerere alikuwa akivikemea ni suala rushwa na kueleza alihakikisha watuhumiwa wa rushwa, walikuwa wakichalazwa bakora 12 wakati wa kuingia jela, na kupigwa bakora 12 wakati wa kutoka jela.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo mkoani Lindi, wakati akihutubia kwenye kilele cha Mbio za Mwenge nchini, iliyoendana sambamba na kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Nyerere.

"Wote mnakumbuka Mwalimu Nyerere alikuwa hapendi rushwa, na yeyote ambaye alijihusisha na vitendo vya rushwa alipigwa bakora kabla ya kutoka na baada ya kutoka jela, kupitia hotuba zake nadhani mnajua hili."amesema Rais Magufuli

"Naikabidhi hii ripoti kwa TAKUKURU ukaikague, uiangalie wale wanaotakiwa kupelekwa mahakamani na wale ambao unaona huwawezi niletee ripoti zao, nataka Tanzania inyooke." amesema Rais Magufuli

Aidha Rais Magufuli amesema Serikali yake imemkumbuka kwa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kujenga viwanda, kutoa elimu bure.