Rais Magufuli alivyolikataa ombi la Kangi

Jumanne , 8th Oct , 2019

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola kushughulikia suala la mgogoro wa familia moja, ambayo iko gerezani kufuatia ugomvi wa familia uliohusisha suala ardhi, na kupelekea mmoja wao kufungwa jela.

Rais Magufuli ametoa maamuzi hayo wakati akzungumza kwenye Mkutano wa Hadhara mkoani Rukwa,  ikiwa ni ziara ya kikazi na kuzindua miradi mbalimbali ikiwemo barabara.

Rais Magufuli amesema "watu wanashtakiana ndugu kwa ndugu unataka Polisi wangu wafanye nini, mtu akienda na Panga kwenye mgogoro wa ardhi OCD afanyaje, OCD wewe fuata sheria, tena nakupongeza, saa nyingine wabaya wanakuja kwako Waziri kumchongea OCD, ila nimuombe ndugu aifute kesi mwenzake ameteseka sana"

Awali Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, aliomba kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya viongozi wa Wilaya, kwa kile alichokilalamikia kuwabambikia kesi baadhi ya wananchi, ambazo ni kinyume na sheria.

"Rais kwa masikitiko kuna viongozi wa Polisi Wilaya, wanageuza kesi za ardhi zinakuwa jinai, kuna familia naifahamu sasa wako gerezani kwa kuonewa na Polisi, naomba uisaidie hii familia, mimi  niliwahamisha hao polisi." amesema Waziri Kangi

Kwa sasa Rais Magufuli anaendelea ziara mkoani Rukwa, ambapo awali alikuwa mkoani Songwe.