Jumanne , 21st Jan , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi 4, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) na Mkuu wa Chuo cha Maji.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli amemteua Prof. Maurice C.Y. Mbago kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Prof. Mbago anashika wadhifa huo kwa kipindi cha pili.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Masatu Masinde Leonard Chiguna kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Dkt. Chiguna anachukua nafasi ya Prof. Ninatubu Mbora Lema ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na bodi kuvunjwa.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Zacharia Mabubu Mganilwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL). Prof. Mganilwa ni Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Mariam Alu Nkumbi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Godwill George Wanga kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC). Kabla ya uteuzi huo Dkt. Wanga alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Adam Omar Karia kuwa Mkuu wa Chuo cha Maji.