Jumatatu , 20th Jul , 2020

Rais Dkt John Pombe Magufuli, amesema kuwa Tanzania imebaki kuwa nchi salama, kwa kuwa ilifanikiwa kutokomeza mbali maambukizi ya Virusi vya Corona baada ya kumtanguliza Mungu na ndiyo maana hata watalii wameendelea kumiminika nchini kwa kuwa wanao uhakika na usalama wa maisha yao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo hii leo Julai 20, 2020, wakati akizungumza na viongozi aliowateua mara baada ya kula viapo Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma.

"Wizara ya Maliasili nimeanza kuona watalii wengi wanakuja, kuna ndege zinaleta watalii wengi, watu wameangalia na wameuona ukweli kwamba hapa Tanzania tuko salama, maadui zetu watazungumza mengi, hata hapa tungekuwa tumevaa barakoa, lakini hakuna aliyevaa hapa ni kwa sababu tuko salama kwani sisi hatuogopi kufa?, lakini Corona iko mbali huko, tuliamua kumuomba Mungu na akatusikia" amesema Rais Magufuli.

Viongozi waliopishwa hii leo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, DC Ilala, Rombo, Maswa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.