Ijumaa , 11th Jun , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Albert Chalamila na kumteua Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi kuwa Mkuu wa mkoa huo.

Albert Chalamila, aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza

Taarifa ya utenguzi huo imetolewa usiku wa kuamkia leo Juni 11, 2021, na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu, zikiwa zimepita siku chache tu tangu Chalamila ateuliwa kuwa Mkuu wa mkoa huo akitokea mkoani Mbeya.

Aidha, Rais Samia amemteua aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Tabora Ally Hapi kuwa Mkuu wa mkoa wa Mara akichukua nafasi ya Mhandisi, Robert Gabriel Luhumbi, aliyehamishiwa mkoani Mwanza.

Sanjari na hayo Rais Samia pia amemteua, Batlida Buriani, kuwa Mkuu wa mkoa wa Tabora, kabla ya uteuzi huo Batlida alikuwa ni Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga.