Jumatano , 23rd Oct , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila ametangaza kuwafukuza Shule wanafunzi saba wa kidato cha sita, waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za kuchoma moto mabweni, katika Shule ya Sekondari Kwanja iliyopo Chunya mkoani Mbeya.

Chalamila ametoa maamuzi hayo leo Oktoba 23, 2019, akiwa Shuleni hapo wakati akitoa ripoti kuhusiana na maamuzi ya kuwatimua wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiwanja wa kidato cha 6 na kuwataka walipe faini ya Shilingi laki 2 kwa kila mmoja, na faini ya Shilingi laki 5 kwa kila aliyechoma moto mabweni.

"Leo Jumanne asubuhi nimewatimua wanafunzi wote ambao hawajalipa, na nitaandika ripoti kwenye mamlaka kuwazuia wasifanye mitihani tena kwa muda wa miaka 5 na kama kuna shule yeyote itawapokea itakuwa hatarini" amesema Chalamila.

"Jinsi ya kuwafuatilia hawa wanafunzi ni ndogo sana, kwa sababu tunawafahamu tangu walipoanzia mpaka wapo sasa na uzuri zaidi tumewalipia ada wenyewe wala hawatusumbui kuwapata, kwa hiyo niseme tu shule yeyote itakayowapokea itakuwa matatizoni" amesema Chalamila.

Hivi karibuni Mkuu huyo wa Mkoa, alionekana kuwashushia bakora baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kiwanja mkoani humo, wakituhumiwa kuchoma moto mabweni ya Shule.