Ripoti ya CAG yazua taharuki kwa Mawaziri

Jumatatu , 16th Apr , 2018

Wenyeviti wa kamati mbili za bunge za hesabu za serikali PAC na ile ya serikali za mitaa LAAC, wamekosoa uamuzi wa baadhi ya Mawaziri waliojitokeza mbele ya waandishi wa habari na kuanza kupangua hoja za CAG kabla hazijafikishwa ndani ya bunge na kudai kitendo hicho ni cha udhalilishaji.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti Naghenjwa Kaboyoka wa PAC na Vedasto Ngombale ambaye ni mwenyekiti wa LAAC, wakati walipokuwa wanazungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Prof. Mussa Assad, kuwasilisha ripoti ya ukaguzi iliyoishia Juni 30, 2017 kwa waandishi wa habari mjini Dodoma wiki iliyopita kisha kuanza kuonekana kwa baadhi ya Mawaziri kujibu ripoti hiyo nje ya Bunge.

"Mawaziri sita ambao wamejibu hoja za CAG kupitia kwa waandishi wa habari wanakiuka sheria na hawapaswi kujibu badala yake wanaotakiwa kufanya hivyo ni makatibu wa wizara wenye wajibu ambao ndiyo wanaitwa na kuhojiwa na kamati husika", wamesema wenyekiti hao.

Hii ni kwa mara ya kwanza katika historia ya bunge nchini, hoja zinazotolewa na CAG zimekuwa zikijibiwa na Mawaziri kabla hazijafikishwa mbele ya Wabunge.