Ijumaa , 19th Jul , 2019

Ripoti ya Mwenendo wa Uchumi wa Tanzania iliyotolewa jana Julai 18, na Benki ya dunia imeleta gumzo mtandaoni baada ya kuonyesha kutofautiana na taarifa ya Serikali iliyotolewa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipnago, Dkt Philip Mpango.

Ripoti ya Uchumi ya Benki ya Dunia yazua gumzo

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, mchumi kutoka Benki ya Dunia, Bill Battaile amesema ripoti ya mwaka huu imeonyesha kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.2 mwaka 2018, ikiwa ni tofauti na ripoti ya Serikali ya Tanzania ambayo imeonesha uchumi wa nchi unakua kwa asilimia 7.

Ripoti ya Benki ya Dunia imeeleza kuwa ukuaji wa kiwango cha uwekezaji, ulishuka kwa sababu ya Serikali kushindwa kuyafikia malengo yake ya matumizi katika miradi ya maendeleo.

Aidha imeshauri kuwa ili kuimarisha uchumi wa nchi, Serikali inatakiwa kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara, ikiwemo kuondoa mabadiliko ya ghafla ya sera yanayosababisha kutotabirika kwa biashara pamoja na kuondoa changamoto kwenye nishati, usafirishaji pamoja na kuboresha miundombinu ya uwekezaji ili kuzivutia sekta binafsi.