Jumapili , 24th Mei , 2020

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, katika kusherehekea sikukuu ya Eid El Fitri, ametoa ofa kwa mtu yeyote atakayelewa kupita kiwango ahakikishe anawasiliana na Jeshi hilo, kwa ajili ya kulichukua gari lake na kulihifadhi na atapaswa kulifuata pale ulevi utakapomwisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana.

Kamanda Shana ameyabainisha hayo, wakati akituma salamu za sikukuu hiyo na kuwataka wananchi wake kusherehekea kwa tahadhari, ikiwemo kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona.

"Natoa ofa pia kama ukijihisi umelewa kupita kiasi wewe tuite, tutachukua gari lako  tutalitunza bure na kilevi chako kikiisha sisi tutakukabidhi, pia tunatoa wito kwa wananchi kuzingatia tahadhari zote za kujikinga na COVID-19" amesema Kamanda Shana.

Aidha EATV&EA Radio Digital, leo pia inawataki Waislamu wote nchini, kusherehekea kwa amani na utulivu sikukuu ya Eid El Fitri, bila kusahau kuzingatia tahadhari za maambukizi ya Virusi vya Corona.