Rukwa: Madhehebu ya dini kupunguza muda wa ibada

Jumanne , 31st Mar , 2020

Viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Rukwa wamekubaliana kuwa kila dhehebu kulingana na imani zao kupunguza muda wa kufanya ibada katika misikiti na makanisa mbalimbali ili kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Rukwa.

Wamekubaliana hayo wakati wa kikao kifupi kilichoitishwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Mh. Julieth Binyura.

Kikao hicho kililenga kuwaelimisha viongozi hao juu ya Chanzo, usambaaji na namna ya kujikinga na ugonjwa huo ambao unaendelea kuisumbua dunia huku jukumu la kutoa elimu likifanywa na Mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa.

Wakati akielezea namna ya kutekeleza azma hiyo Shekhe wa mkoa wa Rukwa Rashid Akilimali alisema kuwa atazungumza na mashekhe wa wilaya na Maimamu wa miskiti ya mkoa huo kupunguza muda wa ibada ili kukwepa kuwaweka watu wengi katika eneo moja kwa muda mrefu lakini pia kuwafanya waumini hao wasikose ibada hizo.

Niungane na Askofu wa Monravian, tupunguze nyakati za ibada zetu, na kubwa iwe ni kuongoza dua na maombi kwaajili ya nchi yetu, sisi tumelipunguza hili baada ya kutokea hili, ibada ya nusu saa tumekwenda dakika kumi na tano, dakika kumi inakuwa ni mahubiri na dakika tano ni kuiombea nchi ili Mungu atuepushe na jambo hili,” amesema Sheikh Akilimali.

Naye Mwakilishi wa Kanisa la Anglikan Mkoani Rukwa Mchungaji Mathias Gwakila amesema, “hicho ni kitu muhimu mno, ibada ziwe fupi zisiwe ndefu, kwahiyo kwa ushauri wangu kupitia madhehebu mengine yote, viongozi wote wa madhehebu wajitahidi kufupiza, kwa mfano kanisa la Anglican ibada zetu ni masaa mawili, sasa tufupishe, ibada ichukue saa moja”.

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, maambukizi ya virusi vya Corona nchini yamefikia watu 19 hivi sasa huku kifo cha mgonjwa mmoja kikitokea leo, Machi 31.