Ruvuma: Walioachiwa kuepusha msongamano wakamatwa

Jumanne , 31st Mar , 2020

Mahabusu walioachiwa kwa dhamana kuepuka msongamano wakati huu wa kusambaa kwa virusi vya Corona wamekamatwa tena baada ya kurejea kwenye uharifu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Marwa Maigwa

Akizungumzia matukio hayo ya uharifu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Marwa Maigwa amesema vitendo vya uharifu vimeongezeka kipindi hiki ambacho taifa linapambana na janga la virusi vya Corona baada ya watuhumiwa waliokuwa na kesi zenye dhamana kutolewa mahabusu sababu ya msongamano wa watu.

"Matukio haya ya uhalifu yanazidi wakati huu ambao nchi inapambana na ugonjwa huu wa virusi vya Corona, kwa vile watuhumiwa wenye makosa yenye dhamana wanaruhusiwa kuepusha msongamano", amesema Kamanda Maigwa.

"Mfano mzuri utaona hawa hawarifu ni wale tuliokuwa tunawashikilia kwa makosa mbalimbali lakini waliachiwa kwasababu kesi zao zina dhamana", ameongeza.

Baadhi ya vitu vilivyokamatwa baada ya msako mkali wa polisi ni pamoja na mashine za EFD, spika za redio, vinywaji pamoja na runinga.