Jumatano , 15th Aug , 2018

Watu watano wamefariki dunia papo hapo na watatu kujeruhiwa, baada ya gari linalodaiwa kuwa lilikuwa likiwakimbia polisi kupinduka, ajali hiyo imetokea jana alfajiri eneo la Mika Kitongoji cha Bukwe wilayani Rorya mkoani Mara.

Pichani gari lililopata ajali.

Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya, Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ajali hiyo ilitokea wakati dereva aliyekuwa amepakia samaki wanaodaiwa kuvuliwa kinyume cha sheria akiwakimbia askari waliokuwa doria.

Baada ya ajali tulikuta mafurushi manne ya samaki yakiwa yameandikwa majina inaonekana ndio, watu waliokuwa wakipelekewa mizigo hiyo na zilichukuliwa na watu wa uvuvi kwaajili ya uchunguzi”, amesema Kamanda.

Mwaibambe amewataja waliofariki dunia kuwa ni mmiliki na dereva wa gari hilo, Athumani Masiaga (42) na Lucia Mwita (27) ambao wote ni wakazi wa Tarime mjini, wengine ni Mang’ala Baruti (40) na Jumanne Makonya (52), wakazi wa mji mdogo wa Shirati wilayani Rorya na Khadija Nangai ambaye umri na makazi yake hayajajulikana.

Kamanda Mwaibambe amewataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Fidelis Fredrick (29), mkazi wa Busurwa wilayani Rorya; Mwita Saitoti (48) na Christina Nyangioso (28) ambao ni wakazi wa Tarime.

Mwezi  Februari mwaka huu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina kupitia oparesheni yake ya siku arobaini aliyoendesha katika mikoa ya kanda ya ziwa kupinga uvuvi haramu, alimwagiza katibu mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia uvuvi Dkt.Yohana Budeba pamoja na wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya katika mikoa ya kanda ya ziwa, kuwafuta kazi mara moja watumishi 65 na viongozi wa kamati za usimamizi wa raslimali za uvuvi (BMU) 26 baada ya kubainika wanashiriki kufadhili uvuvi haramu ndani ya ziwa Victoria.