Jumapili , 24th Mei , 2020

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema kilimo kimeendelea kuwa muhimili katika maendeleo ya uchumi wa Taifa, ambapo katika kipindi cha miaka 5, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, limeongezeka kutoka Sh. Tril. 25.2 Mwaka 2015 hadi Sh. Tril. 29.5 Mwaka 2019.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa upatikanaji wa pembejeo zote za kilimo unakuwa kwa wakati zikiwemo mbegu bora, mbolea sahihi, viuatilifu sahihi na zana bora za kilimo.

Baadhi ya Mikakati ambayo Serikali imeiweka kwa lengo la kuinua kilimo nchini na kipato cha mkulima ni pamoja na kujenga miundombinu ya umwagiliaji,  kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea, kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uongezaji wa thamani ya mazao, kuimarisha mifumo ya uuzaji wa mazao, kuimarisha ushirika, kuimarisha huduma za ugani na mafunzo, kuwekeza katika utafiti wa kilimo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya uhifadhi wa mazao n.k.

Amesema kuwa katika Mwaka huu wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za kilimo (AGITF) imetoa mikopo 93 yenye thamani ya Shilingi 836,359,000 ikiwemo tisa (9) ya mitambo ya mashambani, 80 ya Pembejeo, mmoja (1) wa Ukarabati, miwili (2) ya Miundombinu ya Kilimo na mmoja (1) wa fedha za kuendeshea shughuli za shamba.

Amebainisha kuwa huo ni ushahidi tosha wa nia njema ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwasaidia wakulima nchini ili waweze kuondokana na kilimo duni kisicho na tija.

Sanjari na hilo, Wizara imeendelea kuhamasisha matumizi ya zana bora za kilimo ili kuongeza ufanisi katika shughuli za kilimo. Kutokana na jitihada hizo za Serikali, Wizara kupitia Mfuko wa Pembejeo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 imetoa mikopo mbalimbali  yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 15.1 ambayo kwa pamoja imesaidia kuzalisha ajira takribani 864” Amekaririwa Mhe Hasunga