Serengeti: Wawili wafariki ajali ya ndege

Jumatatu , 23rd Sep , 2019

Watu wawili waliokuwa wamepanda ndege ya mali ya Kampuni ya Auric Air, wamefariki dunia kufuatia ndege hiyo kuanguka katika Uwanja mdogo wa Ndege wa Seronera uliopo kwenye hifadhi ya Serengeti mkoani Mara.

Inadaiwa kuwa watu hao wawili walikuwa wakisafiri kutoka Mara kueleka mkoani Arusha kwa ajili ya shughuli za kitalii, ambapo ajali hiyo imetajwa kutokea leo saa 1:30 Asubuhi.

Mpaka sasa hakuna taarifa kamili juu ya majina ya watu hao wawili waliofariki lakini taarifa mbalimbali zinasema kuwa miongoni mwa waliofariki kwenye ajali hiyo ni pamoja na  mtoto wa Mkuu wa Majeshi Tanzania, Venance Mabeyo, kijana anayeitwa, Nelson Mabeyo.

Juhudi za kumtafuta Mkuu wa Polisi Mkoa wa Mara, bado zinaendelea ili kujua kiundani kuhusiana na chanzo cha ajali pamoja na kutambua miili ya watu waliofariki.