Jumamosi , 17th Dec , 2016

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa amesema Serikali itawanyang’anya ardhi wamiliki wote wa mashamba makubwa wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza, kwa sababu wamekiuka mkataba wa umiliki.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Arumeru akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Arusha ,na kusema serikali haiko tayari kuona wananchi wakinyanyaswa kwa kukosa ardhi ya kilimo kwa sababu ya watu wachache kumiliki maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza.

Waziri Mkuu aliendelea kwa kusema wilaya ya Arumeru inaongoza kwa migogoro ya ardhi na maeneo mengi yametwaliwa na mtu mmoja mmoja, na baadhi yao wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi la Polisi kwa kuwanyanyasa wananchi wanaokatiza au kulima kwenye maeneo hayo.

Awali, akisoma taarifa ya wilaya mkuu wa wilaya ya Arumeru Bw. Alexander Mnyeti, alimweleza Waziri Mkuu kwamba wilaya hiyo ina mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji ambayo hayajaendelezwa, na kuwa kitendo cha kutoyaendeleza mashamba hayo kinasababisha wananchi kuyavamia, hali inayochangia kushamiri kwa migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo.