Jumatano , 16th Mei , 2018

Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One imekubali kuilipa Serikali fidia pamoja na kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali.

Makubaliano hayo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli Profesa Palamagamba Kabudi na  Mkurugenzi wa Tanzanite One Bw.Faisal Juma.

Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa kamati ya majadiliano kwa upande wa serikali, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzanite One imekubali kulipa fidia serikali kutokana na mambo iliyofanya ambayo yalikuwa kinyume na utaratibu ulioleta hasara kwa serikali.

"Fidia hiyo inatakiwa kulipwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza italipwa ndani ya wiki mbili kuanzia leo na haitahusisha kodi. Pia Kampuni hiyo Tanzanite One italazimika kulipa kodi kama kawaida inazodaiwa na serikali na tozo nyingine zote zinazodaiwa na serikali", amesema Kabudi.

Pia serikali imekubaliana na Kampuni ya Tanzanite One kuwa itafuata masharti yote ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kuwa ni watanzania tu ndio wanaoruhusiwa kuchimba madini ya vito na pale ambapo watanzania hawana uwezo huo ndipo wanapoweza kuingia ubia na wageni.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuunda kamati hiyo ya kizalendo katika kufuatilia rasilimali za madini nchini ambapo wameweza kujadiliana na kufikia muafaka wa kulipa fidia ikiwa ni mbali na malipo yote yaliyotakiwa kulipwa serikali ikiwemo kodi.