Serikali yabadili msimamo juu ya elimu ya msingi

Jumatano , 17th Apr , 2019

Serikali imesema kwa sasa hakuna haja ya kubadilisha muda wa kuhitimu elimu ya msingi kwa sababu imebaini muda wa miaka saba unaotumika si kitu kibaya.

Waziri Ole Nasha.

Hayo yamebaisnishwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha leo Aprili 17 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi ambalo limehoji, serikali inazunhgumziaje kuhusu kutotekelezwa kwa sera ya elimu ya kuishia darasa la sita badala ya darasa la saba.

Akijibu swali hilo, Ole Nasha amesema sera siyo msahafu na serikali inaweza kuibadilisha wakati wowote kadri itakavyoona inafaa kwa wakati husika, “Kwa wakati huu tumeona elimu kuanzia darasa la kwanza hadi la saba siyo kitu kibaya. Hatuna haja ya kubadili ndiyo maana tumebakia na mfumo wa zamani”, amesema Ole Nasha.

Ameongeza kuwa, wameanza utaratibu mpya wa udhibiti ubora wa elimu kwa ushirikishwaji ambao unawaleta wadau wote kwa pamoja, pia wanahakikisha waratibu wa elimu wanapata vifaa na ofisi ili kusimamia vizuri kuhakikisha elimu inakuwa bora.