Ijumaa , 20th Apr , 2018

Serikali kupitia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashantu Kijaju, imetolea ufafanuzi tuhuma za upotevu wa pesa takriban trilioni 1.5 zilizotajwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali. (CAG) kwenye ripoti yake.

Akisoma taarifa rasmi Bungeni Dkt, Kijaju amesema kwamba serikali sasa hivi inatumia mfumo mpya wa mahesabu wa kimataifa 'epses acrual', ambao unaweka uwazi mahesabu yote, na umeleta mafanikio makubwa kwa serikali.

Dkt. Kijaju ameendelea kwa kusema kwamba pesa hiyo ilikuwa haijajumuishwa matumizi yake wakati CAG anafanya na kukamilisha mahesabu yake, hivyo hakuna pesa ambayo imepotea bila matumizi yenye taarifa.

Matokeo ya utekelezaji wa mpango mkakati wa uandaaji wa mfumo wa epses acrual excess accruals umeiwezesha serikali na taasisi zake kutoa taarifa za kina, na zinazoonyesha uwazi na uwajibikaji wa taasisi husika, hususani katika usimamizi wa mali, na madeni ya taasisi, kuongezeka kwa uwazi kumewawezesha watumiaji wa hesabu kupata taarifa zinazowasaidia kufanya maamuzi sahihi, na kwa wakati”, amesikika Dkt. Kijau kwenye taarifa hiyo.

Dkt. Kijaju ameendelea kwa kufafanua kwamba ..”Kutokana na matumizi ya mfumo wa huu viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba hakuna fedha taslim ya shilingi trilioni 1.51 iliyopotea, au kutumika kwa matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge, hivyo basi madai ya baadhi ya watu wasioitakia mema taifa letu na serikali yetu ya awamu ya tano, hayana msingi wowote wenye mantiki”.

Taarifa hiyo iliyosomwa na Dkt. Kijaju imesema kwamba taarifa ya CAG imeeleza jumla ya mapato yote ya serikali, kwa mwaka 2016/17, yalikuwa shilingi trilioni 25.3 ambapo fedha hizi zinajumuisha mapato ya kodi, mapato yasiyo ya kodi, mikopo ya ndani na nje, pamoja na misaada na mikopo nafuu kwa mashirika ya maendeleo. Kati ya mapato haya ya 25.3 yalikuwepo pia mapato tarajiwa, kama mapato ya kodi, jumla ya shilingi bilioni 687.3 pamoja na mapato yaliyokusanywa kwa niaba ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya jumla ya shilingi bilioni 203.92.

“Katika uandishi wa taarifa za ukaguzi CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbali mbali ikiwa ni pamoja na taarifa za utekelezaji wa bajeti ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2017, mapato yalikuwa jumla ya shilingi trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa shilingi trilioni 23.79, matumizi haya hayakujumuisha shilingi bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana za hati fungani za serikali zilioiva,. Matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho wakati ukaguzi unaofanyika, hivyo basi, baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia ridhaa za matumizi yalikuwa shilingi trilioni 24. 4, kutokana na ufafanuzi huo shilingi trilioni 1.51 zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi ya serikali yalitokana na mchanganuo ufuatao (angalia katika picha) ”, alisikika Dkt. Kijaju akilielezea Bunge.

Dkt. Kijaju alihitimisha tarifa hiyo akisema kwamba “Napenda kuhitimisha kwamba serikali kupitia wizara ya fedha na mipango imepata mafanikio makubwa sana kwa kutumia mfumo huu wa kimataifa, napenda kulitaarifu Bunge lako na wananchi kuwa serikali ya awamu ya tano ipo makini na haiwezi kuruhusu kwa namna yoyote ile upotevu wa fedha za umma”.