Jumatatu , 10th Feb , 2020

Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefanikiwa kupata amri za kutaifisha mali na fedha zinazohusiana na uhalifu sambamba na fedha zilizolipwa  kutokana na kesi za madini zilizopo katika akaunti ya AFR katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zenye thamani ya Tsh Bilioni 58.6.

Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari leo Jumatatu (Februari 10, 2020) Jijini Dar es Salaam, wakati wa makabidhiano ya utaifishaji wa mali za uhalifu mali hizo baina ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na DPP na Katibu Mkuu Hazina, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga alizitaja mali hizo ni pamoja na Nyumba, magari, viwanja, mashamba, mbao na jahazi.

Mganga alisema Ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, mbali na fedha hizo, imepata amri ya kutaifisha nyumba 24, magari 65, viwanja 9, mashamba 2, mbao 6894, jahazi 1 iliyotokana na uvuvi haramu kwenye ukanda wa bahari kuu ya Tanzania pamoja na boti moja ya Yohanda iliyohusika katika kuingiza nchini vipodozi vyenye sumu.

‘’Kwa ufupi ukuchukua thamani ya madini na kiasi cha fedha zilizomo kwenye akaunti ya Asset Forfeiture Recovery (AFR) ya BOT unapata Tsh 19,639,782,781.46 ambazo nakabidhi, hivyo ukijumuisha thamani ya madini yote, fedha iliyolipwa kutokana na kesi zinazohusiana na madini pamoja na fedha zilizomo kwenye akaunti ya AFR jumla yake inakuwa Tsh 58,604,375,783.56’’ alisema Biswalo.

Biswalo anasema tangu kuzinduliwa rasmi kwa ofisi hiyo mwezi Agosti mwaka 2018, Ofisi yake imefanikiwa kutaifisha jumla ya kilo 397.937 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 32.2 zilizokuwa zikitoroshwa nje ya nchi na kuisababishia serikali kukosa mapato, ambapo kati ya hizo, kilo 351.76 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 29 zimeshakabidhiwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambaye ndiye mtunzaji wa mali za Serikali.

‘’Leo hii nakabidhi jumla ya kilo 46.177 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 3.2, pamoja na hayo tumeendesha kesi na kufanikiwa kupata amri za kutaifisha madini aina ya Almas, Tanzanite, Silver, Amethyst, Rhodolite, Bati, Blue Sapphire, Spinel, Ruby, Tourmaline, Acuamarine, ambapo jumla ya thamani ya madini yote yaliyotaifishwa pamoja na faini zilizolipwa na washitakiwa ni Tsh Bilioni 42.2’’ alisema Biswalo.

Katika hatua nyingine, Biswalo alisema kufuatia marekebisho ya sheria mbalimbali Na. 11 ya mwaka 2019, Ofisi yake imeendesha kesi katika zoezi la washtakiwa kukiri makosa yao ambapo jumla ya Tsh Bilioni 12.3 zimeshalipwa kama kodi iliyokwepwa, faini na  fidia katika akaunti maalum iliyopo Benki Kuu ya Tanzania.