Jumamosi , 16th Feb , 2019

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa serikali imedhamiria kwa dhati kukamilisha mradi mkubwa wa reli kwa kiwango cha kimataifa (SGR), ambapo tayari kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 2 kimetolewa mpaka sasa kwa ajili ya ujenzi huo.

Dkt. Kijaji ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi eneo la Soga, umbali wa kilometa 53, na kujionea maendeleo makubwa ya ujenzi wa reli hiyo.

Ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wake na kumpongeza mkandarasi anaye jenga reli hiyo, kampuni ya Yapi Merkezi, kwa kutekeleza ujenzi huo kwa viwango vya hali ya juu ambapo ameelezwa kuwa, treni ya kwanza kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro inatarajia kuanza safari zake Novemba mwaka huu kama kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.

"Ninampongeza sana Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake kubwa na kuamua kwa dhati kutekeleza mradi huu mkubwa na miradi mingine, ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, ambayo kukamilika kwake kutachochea uchumi wa viwanda" alisema Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Ujenzi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR), kipande cha  kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Mhandisi Machibya Masanja, amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo umekamilika kwa asilimia 42.