Serikali yatoa neno wasiolipwa fedha za korosho

Jumanne , 13th Aug , 2019

Serikali imeendelea kuwapa matumaini wakulima wa Korosho ambao bado hawajakamilishiwa malipo yao na kuwataka kutokata tamaa, kwani tayari wanunuzi wamepatikana korosho zote zilizopo ghalani zitanunuliwa ndani ya muda mfupi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba alipokuwa akifunga maonesho ya 27 ya wakulima Nane-Nane Kanda ya kusini, katika viwanja vya Ngongo vilivyopo katika Manispaa ya Lindi.

Naibu Waziri Mgumba amesema wakulima hawana sababu za kukata tamaa wa kutolipwa fedha zao za korosho, kwani bado uhitaji wa zao hilo Duniani ni kubwa na tayari wanunuzi wa kuzinunua wamepatikana.

"Nachukuwa nafasi hii kuwaelezeni kwamba Korosho zote zilizopo maghalani kuanzia kusini hadi Dar es salaam zimepata wanunuzi. Kufuatia ubora wa Korosho zetu ulivyo, upo uhakika mkubwa bei ya zao hili kwa mwaka huu ukawa mzuri zaidi", amesema Naibu waziri Mgumba.

Naibu Waziri huyo wa Kilimo amekanusha taarifa zinazoendelea kutolewa kwamba korosho zilizopo kwenye maghala kwamba zimeoza, huku akiwataka wananchi kupuuza madai hayo, kwani wanunuzi wamepitishwa na kuzikagua na kubaini ni mzima.